Kasi ya ufungaji ya kiungo mshambuliaji wa Simba Shiza Kichuya kama imepungua hivi ukilinganisha na msimu uliopita ambao alikuwa anafunga kadiri anavyotaka. Msimu uliopita 2016/17 Kichuya alimaliza akiwa na zaidi ya magoli 10 akikimbizana na wafungaji bora wa msimu huo Simon Msuva na Abdulrahman Musa. Msimu huu hadi sasa zikiwa zimechezwa mechi 17 Kichuya anamagoli sita, kuna baadhi ya maswali yameanza kuulizwa kwa nini kiungo huyo ameshuka kiufungaji.
Kichuya amejitokeza na kutaja sababu zinazomfanya asifunge kama ilivyokuwa msimu uliopita, amesema amebadilishiwa majukumu na benchi la ufundi hivyo anatakiwa kuwafanya washambuliaji wafanye kazi yao lakini pia hafungi kuwaridhisha watu atafanya hivyo ikiwa yupo kwenye nafasi ya kufunga.
“Watu wanatakiwa kujua kwenye mpira kila mchezaji ana nafasi yake ambayo anaweza kuitendea haki kadiri ya uwezo wake, kwa sasa kwenye timu yetu kila mtu anaitendea haki nafasi yake ambayo anacheza, ukiangalia nafasi ya washambuliaji kila wakipata nafasi wanafunga na sisi viungo ndiyo tuna kazi ya kubwa ya kutengeneza hizo nafasi ili kuwafanya kila siku waonekane bora.”
“Watu hawatakiwi kushangaa kwa nini msimu huu sifungi kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa sababu kila msimu una mambo yake halafu kila mwalimu anakuwa na mbinu zake sasa hivi nimepewa maelekezo ya kuwatengenezea zaidi wenzangu kwa ajili ya kuifanya timu nima ionekane bora kwa hiyo siwezi kung’ang’ania kufunga hata kama sipo kwenye nafasi ya kufunga kwa sababu ya kuwaridhisha watu wanaosema sikuhizi sifungi.”
“Ninachokifanya sasa hivi ni kuangalia namna gani timu inapata matokeo na nini ambacho wanasimba wanakihitaji kwa sasa kwa sababu hakuna kitu chochote kinachoweza kuwafanya wakatuelewa isipokuwa ni ubingwa kwa hiyo wachezaji, benchi la ufundi tunafanya kitu ambacho wanasimba wanataka.”
Jumapili hii Februari 11, 2018 Simba itarejea kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya kimataifa baada ya kuikosa kwa misimu mitano mfululizo, Kichuya wala hana presha anasema kwa sababu ameshacheza mechi nyingi za kimatifa kwa hiyo haitakuwa jambo jipya sana kwake.
“Nimeshacheza mechi nyingi za kimataifa kwa hiyo sidhani kama mchezo huu utanipa changamoto kubwa sana kinzchotakiwa sasa hivi ni mimi kujua tunakwenda kushinda katika ngazi gani, mchezo huo sio wa ligi kuu , kitu nachotakiwa kufanya ni kuijitofautisha na Kichuya wa mechi za bongo.”
Neno la Kichuya kwa mashabiki wa Simba kuelekea mchezo wao wa kimataifa: “Waje kwa wingi na sisi wachezaji kwa jitihada zetu na maelekezo ya mwalimu tutafanya kitu ambacho kimewafanya waache kazi zao kuja kutuangalia sisi, hatutawaangusha.”
No comments:
Post a Comment